Urusi imeanza mazoezi ya kijeshi katika eneo la kusini mwa taifa hilo, sambamba na katika maeneo yaliyojitenga na Georgia ya Ossetia Kusini, Abkhazia na Crimea ambayo ilijiunga na Urusi mwaka jana kutoka Ukraine. Taarifa hizi zimetolewa na shirika la habari la Urusi RIA ambalo limeinukuu Wizara ya Ulinzi ya Urusi.
Na huku Ukraine, waziri wa fedha wa Ukraine Natalie Jaresko amesema nchi hiyo itaanza mazungumzo na wakopeshaji wake yanayolenga kulifanyia mageuzi deni lake.Kwa mujibu wa msemaji wa waziri huyo mazungumzo hayo yanatarajiwa kuanza kesho. Hata hivyo Jaresko hakufafanua mkopo gani hasa utafanyiwa marekebisho hayo. Mataifa yanayoidai Ukraine ni pamoja na Urusi inayomiliki dhamana za thamani ya dola bilioni 3, kati ya jumla ya dhamana za thamani ya dola bilioni 17 zilizotolewa na serikali ya Kiev. Lakini pia wachambuzi wanasema mikopo kutoka katika mabenki ya kigeni na serikali vilevile inawezwa kulengwa. Tangazo hilo limetolewa siku moja baada ya shirika la fedha duniani IMF kuidhinisha kiasi cha mkopo wa dola bilioni 17.5 katika taifa hilo lenye ukosefu mkubwa wa fedha ili kulisadia lisishindwe kabisa kuyalipa madeni yake.